Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa mamlaka ya ukaguzi wa hesabu kwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini mwelekeo mpya unaonyesha Wizara ya Fedha inamhakiki pia CAG.
Mwelekeo huo uko katika majibu ya Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji alipoliambia Bunge kwamba Serikali itakuwa tayari kulipa madeni yote inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kukamilisha uhakiki.
Kauli hiyo ni kinyume cha Ibara ya 143 ya Katiba inayompa CAG mamlaka ya mwisho ya ukaguzi na kuwasilisha ripoti yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kifungu (1) kinasema kutakuwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano.
Majukumu yake yameainishwa katika kifungu (2) kinachosema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu atakuwa na jukumu juu ya mambo yafuatayo: (a) kuhakikisha kwamba fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali matumizi yake yameidhinishwa na kwamba zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya Katiba hii, na iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe.
Kifungu (c) kinamtaka angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za Mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na hesabu zinazosimamiwa na Katibu wa Bunge.
Aidha, Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na 11 ya mwaka 2008 imempa CAG mamlaka ya mwisho na kwamba hawezi tena kukaguliwa.
Alipoulizwa CAG, Profesa Mussa Assad kuhusu nani anapaswa kumhakiki baada ya kufanya ukaguzi alisema ofisi yake ina mamlaka ya mwisho.
“Tukishakagua sisi Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali hakuna chombo kingine kinachorejea ukaguzi, kazi inakuwa imekwisha,” alisema.
Profesa Assad aliulizwa swali hilo kufuatia hatua ya Serikali kusema kwamba inafanya uhakiki wa madeni yote ya mifuko ya hifadhi ya jamii kabla ya kulipa. “Serikali italipa malipo yote ikikamilisha uhakiki,” alisema Dk Kijaji.
Dk Kijaji alisema hayo alipokuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia maoni yao katika hotuba ya Bajeti ya mwaka 2016/ 17 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philipo Mpango. Wabunge walihoji kwa nini Serikali hailipi deni la mifuko ya hifadhi za Jamii linalofikia takriban Sh8.94 trilioni.
Dk Kijaji alisema wanaendelea kuhakiki madeni hayo kwa sababu wamebaini yapo madai hewa na kwamba mapitio ya awali yameonyesha madai yamefikia Sh3.89 trilioni hadi Juni 2015 likihusisha deni la Mfuko wa Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF) la kabla ya mwaka 1999 ambalo ni Sh 2.67 trilioni na Sh 1.22 trilioni kwa ajili ya madai ya mifuko yote yaliyotokana na uwekezaji wa miradi mbalimbali ya serikali.
“Serikali italipa malipo yote ikikamilisha uhakiki. Mfano, Mei 2016 uhakiki wa madai ya PSPF ulikuwa umekamilika na madai yaliyokubalika ni Sh2.04 trilioni kutoka madai ya Sh2.67 trilioni, hii inaonyesha kuwa kulikuwa na madai ya wastaafu hewa,” alisema Dk Kijaji maelezo yanayoonyesha kwamba CAG katika ukaguzi wake hakubaini wastaafu hewa.
Hata hivyo, alipoulizwa kama kwa kufanya uhakiki Serikali haiendi kinyume na mamlaka ya CAG ambaye kisheria ndiye mkaguzi wa mwisho, Dk. Kijaji alijibu, “Siyo kweli, labda tu kama hukunielewa…tafuta taarifa sahihi.”
Ripoti ya CAG kuhusu deni la Serikali kwa PSPF ilisema mfuko huo una hasara ya thamani ya Sh11.15 trilioni kwa mwaka 2014 na Sh6.49 trilioni kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika mwaka 2010.
Profesa Assad alisema kuwa msingi wa hasara hiyo ni matokeo ya Serikali kuchelewa kulipa madeni ya mafao ya wanachama waliokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa mfuko Julai Mosi mwaka 1999.
Alisema katika ripoti hiyo kuwa mfuko wa PSPF una madai ya mikopo kutoka taasisi za Serikali yenye thamani ya Sh499.7 bilioni kufika Juni 30 2015.
Mwaka 2008 wakati inaundwa Sheria ya Ukaguzi wa Umma ulizuka mjadala kwamba Waziri wa Fedha amkague au ateua mtu wa kumkagua CAG lakini iliamliwa kwamba mkaguzi huyo awe na mamlaka ya mwisho kisheria.
Jiunge na BONGOHOTZ.COM sasa
Usipitwe!! kupitia FACEBOOK, TWITTER naINSTAGRAM kupata habari ndani ya sekunde kila inapotufikia..!! Usiache ku download application play store BOFYA HAPA KU DOWNLOAD....... LIKE PAGE YA BONGOHOTZ KWENYE FACEBOOKLIKE PAGEDOWNLOAD APP YA "BONGOHOTZ" UPATE NOTIFICATION KWA KILA KITU KIPYA
Post a Comment