today news

DC KINONDONI ATUA MWANANYAMALA HOSPITALI


*Abaini gharama ya kadi ya wagonjwa kupandishwa hadi 10,000/= bila kufuata utaratibu
 
*Aagiza kusitishwa mara moja

*Mganga mfawidhi kuchukuliwa hatua

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi leo asubuhi amefika katika hospitali ya Mwananyamala akiambatana na Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni na mganga Mkuu wa Kinondoni. Hapi amefika hospitalini hapo na kuongoza moja kwa moja kwenye dirisha la malipo ambapo imebainika kuwa gharama za kadi ya mgonjwa zimepandishwa bila kufuata utaratibu na kufikia shilingi 10,000 kwa mgonjwa kumuona daktari.  
Hapi ameyabaini hayo licha ya taarifa ya uongo iliyotolewa na msimamizi wa dirisha la malipo kuwa wamesitisha kutoza kiasi hicho .

Mkuu huyo wa wilaya alimuagiza mtaalam wa Max Malipo kufungua kompyuta yake na kuangalia ni kiasi gani ambacho wagonjwa waliofika saa 1 asubuhi leo walitozwa. Baada ya mtaalam huyo wa Max Malipo kufungua ikabainika kuwa wagonjwa wote walitozwa shilingi 10,000/=.

"Hivi wewe dada kwanini ulikua unanidanganya? Unadhani mimi ni mjinga? Unadhani nimekuja hapa kwa bahati mbaya? Najua kila kitu mnachofanya hapa. Ndio maana nikaitwa Mkuu wa Wilaya. Usirudie kunidanganya tena..." alisema Mh Hapi.

Baada ya kuzungumza na wagonjwa walioeleza kilio chao kuwa bei za vipimo pia zimepandishwa kinyemela, mkuu wa wilaya ameagiza Mkurugenzi na mganga mkuu kupitia maamuzi yote ya upandishwaji wa gharama bila kufuata utaratibu na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili watu masikini wasishindwe kupata huduma.

"Wananchi masikini hawawezi kumudu gharama ya shilingi 10,000/= kwa kadi. Hii ni hospitali ya serikali na sio binafsi. Naagiza utaratibu ufuatwe na bei hii isitishwe kutumika mara moja. Badala yake bei ya awali iendelee. Huu ni uchonganishi mkubwa unaolenga kuwafanya wananchi waichukie serikali yao. Hatuwezi kuvumilia."

Naye Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni bwana Aron Kagurumjuli alieleza kuwa tayari amechukua hatua ya kumvua wadhifa wake mganga mfawidhi wa hospitali ya Mwananyamala kuanzia leo hii. 

Gharama mpya za daktari kuona mgonjwa zinatajwa kupandishwa kutoka shilingi 6,000 hadi 10,000/= kwa mgonjwa kuanzia tarehe 1 Ogasti mwaka huu.
Post a Comment

Post a Comment