Mtoto Bahati John mwenye umri wa miaka minne na nusu amefariki dunia na vifaa vya ndani ambavyo thamani yake haijajulikana kuteketea moto.
Tukio hilo limetokea saa kumi jioni katika mtaa wa Kamachumu, Kata ya Kirumba wilayani Ilemela jijini Mwanza.
Kamanda wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Mussa Kaboni amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni jiko la mchina lililowashwa bila kufuatiliwa na muwashaji.
Amesema kuwa katika tukio hilo, wakati wahusika wanawasha jiko hilo kulikuwa na watoto wawili Emmanuel John na Bahati John ambao walikuwa wamelala ambapo mkubwa wao Sospeter aliyekuwa anatoka shuleni ndiye aliwemwokoa mdogo wake mmoja Emmanuel.
“Chanzo ni moto uliosababishwa na jiko la mchina ambalo liliwashwa bila kufuatiliwa, sisi tulipigiwa simu na kufika, lakini bahati nzuri tumekuta wasamaria wameshazima moto na kuokoa baadhi ya vitu,”amesema.
Mzazi wa marehemu, Lulu John amesema alipata taarifa akiwa kazini na alipofika alikuta mwanaye ameshafariki na baadhi ya vitu kuungua.
“Hii ni tabia yake mfanyakazi kuacha jiko linawaka anakwenda zake,”amesema John.
Diwani wa Kirumba, Alex Ngussa amewataka wazazi na walezi kuwa waangalifu wanapokuwa kwenye shughuli za mapishi.