Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.
Serikali imesema uchunguzi wa awali wa vifo vya watu wanane mkoani Dodoma umeonyesha kuwa vilitokana na familia kula ugali wa unga wa mahindi wenye sumu kuvu B (aflatoxins B).
Jeshi la Polisi lilizuia mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya mkoani Dodoma ambao ni wafuasi wa Chadema yaliyokuwa yafanyike kwenye hoteli ya African Dream, likisema mikusanyiko yote imezuiwa baada ya kuzuka ugonjwa usiojulikana ambao awali uliua watu sita.
Wakati Jeshi la Polisi likizuia mahafali hayo ya Chadema, taasisi nyingine zilikuwa zikiendelea na mikutano kwenye hoteli hiyo, jambo lililowafanya viongozi wa Chadema kulalamikia hafla yao kusambaratishwa na polisi waliokuwa na silaha za moto na gari la maji ya washawasha.
Mbali na kuongezeka kwa idadi ya waliofariki dunia, watu waliougua ugonjwa huo wameongezeka kutoka 21 hadi 28.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Khamis Kigwangalla alisema pamoja na matokeo hayo ya awali, watalaamu wengine wa afya walienda wilaya za Chemba na Kondoa kuchukua sampuli nyingine.
Alisema wataalamu hao wanatoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Alisema sumu kuvu inatokana na fangasi wanaokuwa katika mazao ya nafaka au mahali ambapo mazao hayo yamehifadhiwa.
Hata hivyo, alisema athari za sumu kuvu hizo ni za muda mrefu na inamuweka mtu katika hatari ya kupata saratani ya ini.
Dk Kigwangalah alisema uchunguzi huo umethibitisha kuwa ugonjwa huo si Homa ya Bonde la Ufa wala manjano, ingawa baadhi ya dalili zinafanana.
Jumapili iliyopita Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema wamechukua hatua mbalimbali ikiwamo kuchukua sampuli za maabara kwa ajili ya utambuzi wa ugonjwa na damu, mkojo, kinyesi, matapishi na vinyama vinavyotokana na ini vimechukuliwa. “Sampuli zote zimepelekwa Maabara ya Taifa, Mkemia Mkuu wa Serikali na Maabara ya Kilimanjaro Christian Research Institute (KCRI) iliyopo Kilimanjaro kwa uchunguzi zaidi,” alisema.
Post a Comment