Hotuba ya Ndg. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb Kigoma Mjini katika Bajeti ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Wanawake na Wazee
Afya imepewa 3% tu ya Bajeti, Huduma za Sickel cell zasimamishwa Muhimbili, Watoto wapoteza maisha. Azimio la Abuja 15% ya Bajeti ya Afya, Tanzania yatenga 3%
Mheshimiwa Spika, Kazi ya kwanza aliyofanya Rais John Magufuli katika siku zake za mwanzo kabisa Ofisini ilihusu Wizara ya Afya. Alitembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutoa maagizo mbalimbali kuhusu Afya. Tuliona baadaye watendaji wakuu wa Wizara wakihangaika huku na kule kutekeleza maagizo ya Rais. Wengi tulitaraji kuwa Afya za wananchi yetu zitakuwa kipaumbele kikubwa kabisa kwa Serikali.
Hata hivyo ukitazama Bajeti ya Wizara ya Afya yenye jumla ya Shilingi 845 Bilioni sawa na 3% ya Bajeti ya 2016/17 unakata tamaa. Serikali inaweza kusema kwamba Bajeti imeongezeka kwa tarakimu lakini kimsingi imeongezeka kwenda chini ( in decreasing order ) kwani mwaka 2015/16 Bajeti ya Wizara ilikuwa 2% kulinganisha na asilimia 3% za mwaka huu. Nyongeza ya asilimia 1 ni ‘negligible’ (si Kitu Kizito) kabisa hasa ukizingatia kuwa thamani ya shilingi imeporomoka sana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Mheshimiwa Spika, chukulia mfano wa Madawa ( essential medicines ) ambapo Serikali imepanga kutumia tshs 251 bilioni mwaka 2016/17 kwa Bohari ya Madawa, lakini katika fedha hizo tshs 131 bilioni ni za kulipa madeni ya miaka ya nyuma. Kimsingi Bajeti ya madawa ya mwaka huu ni tshs 120 bilioni tu.
Serikali ilitangaza kuwa Deni la MSD limehamishiwa Wizara ya Fedha, imekuwaje limerejeshwa Wizara ya Afya? Napendekeza kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya madawa mwaka huu zitumike kwa madawa na deni la miaka ya zamani la MSD liende Wizara ya Fedha kama ilivyokuwa imeamuriwa miaka 2 iliyopita. Wananchi wetu wanaumizwa sana na ukosefu wa madawa ya msingi.
Utafiti na Huduma za sickle cell Hospitali ya Muhimbili
Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa Bajeti miradi yetu mingi imekuwa ikitegemea wafadhili na hivyo wafadhili wanapojitoa miradi hufa. Miradi ya Wizara ya Fedha inaposimama ina maana maafa ya watu wetu. Kwa mfano, kwa takribani miaka 10 Taasisi ya Wellcome Trust ilikuwa inafadhili utafiti na huduma za clinic ya ugonjwa wa Sickle Cell katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Clinic hiyo ilikuwa inaendeshwa na Daktari mwenye nishani za Kimataifa ( Royal Society Pfizer Award ) Dkt. Julie Makani. Wafadhili wamejitoa katika mradi huu kutokana na maamuzi ya Serikali ya Uingereza kupunguza fedha za misaada ya maendeleo na hivyo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imesimamisha huduma za ugonjwa wa sickle cell. Hospitali ya Muhimbili sasa inawarudisha watoto wote wenye sickle cell kwenda hospitali za Mikoa ambazo hazina huduma hii, hazina clinic hizi.
Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya Nne Duniani kwa kuzaa watoto wenye sickle cell baada ya Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na India. Hivi sasa Tanzania ina watoto takribani 12,000 wenye sickle cell. Tangu Serikali iliposimamisha huduma ya sickle cell katika hospitali ya Muhimbili, mwanzoni mwa mwaka huu, watoto Watatu (3) tayari wamepoteza maisha kwa kukosa huduma.
Mheshimiwa Spika, Serikali inayojali wananchi wananchi wake haiwezi kamwe kukubali watoto 12,000 nchini wakose huduma. Serikali inapaswa kuendeleza clinic hii kwa kutumia fedha za ndani. Kimsingi Serikali ilitamka kutenga fedha za Utafiti sawa na 1% ya Pato la Taifa. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ipewe sehemu ya fedha hizi ili kuendelea na huduma ya sickle cell. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ifanye mazungumzo na Dkt. Julie Makani ili kuona namna bora ya kurudisha huduma hii.
Damu salama
Mheshimiwa Spika, tatizo kama hilo lipo pia kwa hifadhi ya Damu salama. Wafadhili wamejitoa kwenye mradi lakini Serikali haitengi fedha kwa ajili ya Damu salama na matokeo yake Wananchi hawapati damu. Serikali itenge fedha kwa ajili ya kununulia vitendanishi na upatikanaji wa Damu salama kwa wananchi wetu.
Kichwa Kikubwa
Mheshimiwa Spika, hivi sasa kuna kampeni inayoendelea ya upasuaji wa watoto wa kichwa kikubwa na mgongo wazi Nchi nzima. Ubunifu uliofanywa na Dkt. Othman Kiloloma kwa kupata msaada kutoka GSM Foundation unasaidia kwa sasa. Lakini kama Serikali haijipangi maana yake ni kwamba mfadhili huyu akitoka na mradi utakufa. Napendekeza Serikali itazame miradi hii muhimu ili iwe inatengewa fedha kwenye Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, nashauri Bajeti ya Wizara ya Afya iongezwe mpaka kufikia angalau tshs 1.2trn au 5% ya Pato la Taifa ili kuweza kukidhi mahitaji ya huduma za Afya kwa Wananchi. Huduma za Afya maeneo ya vijijini yatiliwe mkazo zaidi kuliko mijini.
Uhaba wa watumishi wa Afya
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa sana la uhaba wa watumishi katika sekta ya Afya. Zahanati nchini zina uhaba wa Wataalam wa maabara Kwa 93%, wauguzi wa ngazi ya cheti Kwa 65% na maafisa tabibu Kwa 52%. Vituo vya Afya vina uhaba wa wauguzi wa ngazi ya cheti Kwa 65% na Hospitali za Wilaya zina uhaba wa wauguzi Kwa 77% na uhaba wa madaktari Kwa 74%.
Uhaba huu unatisha kiasi cha kupelekea Baadhi ya wahudumu wa afya kufanya kazi za maafisa tabibu. Nilipotembelea kituo cha Afya cha Dutwa Wilaya ya Bariadi nilikutana na Mama mhudumu wa Afya aliyefanya kazi kama mfawidhi wa Zahanati kwa miaka zaidi ya Mitatu (3). Kuna maeneo walinzi wa Vituo vya Afya wanatoa huduma kama waganga. Hali hii haiwezi kuendelea. Ni lazima kuwapa huduma bora wananchi kwa kuhakikisha tunaajiri watumishi kwa mujibu wa ikama.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya ina kibali ncha kuajiri watumishi wa Afya na mpaka Mwezi Mei 2016 hakuna aliyeajiriwa na vibali vya ajira vinamaliza muda wake ifikapo mwisho wa Mwezi Juni 2016. Kama ilivyopendekezwa kwenye Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya iongeze uzalishaji wa idadi ya wataalam hususan matatibu, wataalam wa maabara na wauguzi.
Mikoa ya pembeni na pembezoni mwa nchi inapata shida sana ya watumishi wa Afya. Kwa mfano katika Mkoa wa Kigoma na hususan Jimbo la Kigoma Ujiji baadhi ya zanahani hazina kabisa matabibu wala wauguzi. Serikali haitaweza kamwe kuleta maendeleo ya Viwanda bila ya kuhuisha siha za wananchi. Afya na Elimu ni sekta ambazo lazima ziimarishwe ili kuwa na Uchumi wa Viwanda, vinginevyo hivyo viwanda vitajengewe watu wengine na sio Watanzania.
Bodi ya Kitaaluma ya Fiziotherapi
Mheshimiwa Spika, Jambo jingine linalohusiana na Afya ninalopendekeza ni uanzishwaji wa Bodi ya Wataalamu ya Fiziotherapi. Taaluma hii haina Bodi na hivyo usajili wa wataalamu hawa na utoaji wa leseni za uendeshaji wa huduma yao hauna uratibu mzuri na matokeo yake huduma zimekuwa zikitolewa na watu wasio na taaluma na hata kupelekea mmomonyoko mkubwa wa maadili. Serikali ichukulie uzito kilio cha siku nyingi cha Wataalamu wa Fiziotherapi kwa kuanzisha Bodi yao ya Usajili na Leseni.
Bima ya Afya kwa wote
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni kuhusu Bima ya Afya kwa Watanzania wote. "Health care financing" katika nchi yetu bado ni changamoto kubwa sana na hivyo kusabibisha huduma za afya kwa wananchi wengi kuwa za kubahatisha.
Mfumo wa ‘healthcare financing’ una maeneo matatu makuu – ukusanyaji wa mapato, ‘risk pooling’ na manunuzi. Kila mwaka tunatenga fedha nyingi sana kwa ajili ya manunuzi ya madawa na vifaa tiba jambo ambalo kama tungeweza kuwa na mfumo madhubuti wa Bima ya Afya lisingekuwa ni tatizo kubwa sana maana nguvu za soko na usimamizi tu wa Serikali zingeweza kufanya kazi hiyo kwa ufasaha sana. Serikali inaongelea "Universal Health Insurance" lakini mpaka sasa hatujaonanhatua madhubuti za kuelekea huko.
Mheshimiwa Spika, mfumo wetu wa Bima ya Afya haujaratibiwa vizuri na matokeo yake kuna watu kimsingi wanalipia bima za Afya mara 2 kutokana na kukosekana kwa uratibu. Hivi sasa kwa mfano kuna skimu za bima ya Afya za kitaifa kama NHIF na CHF na vile vile fao la Afya kutoka NSSF. Siku za karibuni PSPF na PPF wameanzisha Fao la Afya pia kwa wachangiaji wao wa hiari. Hata hivyo, Shirika la ILO ambalo Tanzania ni mwanachama limeainisha mafao 9 kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na moja ya hilo ni Fao la Bima ya Afya. Kwa hiyo katika kila mchango wa Mfanyakazi kwa mfano, kuna asilimia ya mchango inakwenda kwenye huduma ya Afya. Hata hivyo, ukiachana na NSSF mifuko mingine haifanyi hivyo na matokeo yake Wafanyakazi, hasa Wafanyakazi wa Serikali wanajikuta wanakatwa 20% kwenda kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii na pia wanakatwa 6% kwenda Mfuko wa Bima ya Afya. Hii si Sawa, Ni kuwaumiza Hawa Wafanyakazi Wanyonge.
Mheshimiwa Spika, mapendekezo yangu ni kwamba Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii Nchini iwe inapeleka michango ya Wanachama wao NHIF ili kuwe na Mfuko mmoja tu wa kitaifa. Kwa hiyo, kutokana na mahesabu ya kiakchurio ( actuarial ), % ya michango inayopaswa kuwa ya Afya kutoka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe remitted NHIF na hivyo kila Mtanzania ambaye anakuwa ni Mwanachama wa Mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii anakuwa ,moja kwa moja ni mwanachama wa NHIF.
Kwa maana hiyo SHIB ya NSSF iunganishwe na NHIF na Wafanyakazi wa Serikali wasikatwe tena 6% kwenda NHIF bali PSPF, LAPF,PPF na GEPF iremit sehemu ya michango ya wanachama wao kwa NHIF. "A unified Health Insurance Scheme" inaweza kuwa chachu ya kuelekea Universal Health Insurance coverage.
Kigoma na Ruangwa
Mheshimiwa Spika, katika Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Wilaya Ruangwa kuna mradi wa majaribio ya kuwafanya wananchi wajiwekee akiba kupitia mfuko wa NSSF na Kisha kupata Bima ya Afya kama Fao. Mradi huu wa miaka mitano utawezesha Halmashauri hizi 2 nchini kuwa na "Universal Health Insurance coverage" katika kipindi cha miaka Miwili (2) inayokuja.
Wizara ya Afya ifuatilie kwa karibu mradi huu ili iweze kuona kama kuna mafunzo katika juhudi za kuhakikisha Watanzania wote wanakuwa na Bima ya Afya.
Nawasihi Wabunge wengine wafuatilie tunachofanya Kigoma Ujiji na Ruangwa ili kuona namna bora ya kufikisha huduma za Afya Kwa Wananchi wa majimbo yetu.
Ninaamini kabisa kwamba hata mradi wa tshs 50m kila kijiji ukitumika vizuri unaweza kuwa kichocheo kikubwa kwa wananchi wetu kuweka akiba, kupata bima ya afya na hata kupata mikopo kupitia vikundi vyao vya Ushirika.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha
Ndugu Zitto Zubeir Ruyagwa Kabwe
Mbunge Kigoma Mjini (ACT Wazalendo)
Mei 12, 2016
Post a Comment