NAKUKARIBISHA mpenzi msomaji kwenye ukurasa huu mzuri. Wiki iliyopita tuliianza mada ya… lakini kwa bahati mbaya, nalazimika kuikatisha mpaka baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo tutaendelea. Kwa wale ndugu zangu ambao wapo kwenye mfungo, basi nawatakia mfungo mwema lakini leo ningependa zaidi kuzungumza na ndugu zangu wa upande wa pili, hususan wanawake. Jamii ya Kitanzania imejengwa katika msingi wa kupendana, kuheshimiana na kuishi kama ndugu wa baba na mama mmoja. Duniani kote inafahamika kwamba sifa ya Watanzania ni ukarimu, ucheshi na amani.
Kama ni hivyo, sote tunafahamu kwamba huu ni Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo Waislam nchini wanaungana na wenzao duniani kote katika mwezi huu wa toba na kumrudia Mungu. Yawezekana wewe si Muislam kwa sababu Tanzania ina watu wenye imani tofauti, wapo Wakristo, Wabudha na dini nyingine nyingi lakini pia wapo Wapagani. Haimaanishi kwamba kama wewe si Muislam basi mwezi huu wa Ramadhani haukuhusu kabisa. Lazima wapo ndugu, jamaa, marafiki au hata majirani zako ambao ni Waislam, na wamefunga.
Sasa ili kuwarahisishia funga yao, ni muhimu kila mmoja wetu akawa makini ili asimkwaze mwingine. Unakuta mwanamke anajua kabisa kwamba wenzake wapo kwenye mfungo lakini kwa sababu yeye si wa dini hiyo, basi haoni hatari kuvaa kihasara mchana wa jua kali, anaonesha maungo yake yasiyostahili kuonekana, anatembea mitaani bila hata wasiwasi! Hapana, hii si sawa.
Wewe hujafunga, sawa! Lakini vipi kuhusu ndugu zako, vipi kuhusu marafiki zako, vipi kuhusu majirani na watu wengine waliopo kwenye mfungo? Kwa nini uwe sehemu ya majaribu kwa watu waliopo kwenye toba? Tunajua sote kwamba majaribu ni mtaji wa shetani. Kwa nini ukubali kuwa wakala wa shetani?
Unaweza kupendeza bila hata kuacha sehemu kubwa ya kifua chako wazi. Unaweza kupendeza bila kuvaa nguo iliyokubana na kuchora makalio yako au shepu yako. Unaweza kupendeza bila kuanika mapaja yako wazi! Jistiri japo kwa muda mfupi uwape ahueni waliopo kwenye mfungo.
Kwa nini unawapa wenzako tabu ya kutembea wakiwa
wametazama chini au wametazama pembeni wakikwepa kuuona ulimbukeni wako wa kutembea nusu utupu wakati unajua huu ni mwezi wa toba? Kwa nini unalazimisha wengine washinde ndani tu wakikwepa kuharibu swaumu zao kwa kujikuta tamaa zimewaka kwenye miili yao kwa sababu ya makusudi yako ya kutembea ukiwa umevaa kihasara? Uungwana ni vitendo, hebu onesha uungwana wako kwa siku hizi chache tu za mwezi mtukufu kisha baada ya hapo, ruksa kuendelea na life style yako.
Hata kama huna mazoea ya kuvaa kiheshima, hebu basi jaribu kujistiri kwenye kipindi hiki ili usitumike na shetani kuharibu ukaribu wanaoujenga wenzako kwa mola wao. Ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri, hasa zinazohusu mwezi mtukufu na mfungo.
Post a Comment