Wakati wabunge wa Ukawa wakiendelea kususia vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai anakusudia kuwasilisha kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ombi la Ukawa la kumng’oa naibu huyo.
Hatua hiyo ya Spika imekuja baada ya Mbunge wa Simanjiro, James Kinyasi Millya kuwasilisha taarifa ya kusudio la kuleta bungeni hoja ya kumwondoa madarakani Dk Tulia, Juni Mosi mwaka huu.
Taarifa iliyoletwa kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Bunge, ilieleza kuwa utaratibu huo ni wa Kikatiba na upo chini ya Ibara ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ambapo pia umeainishwa katika Kanuni ya 138 (1), ya kanuni za kudumu za Bunge kuhusu utaratibu wa kumwondoa Naibu Spika madarakani.
“Baada ya kupokea kusudio hilo, Kanuni za Bunge zinamtaka Spika kuiwasilisha hoja hiyo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ifanyiwe kazi.” Ilisema taarifa hiyo.
Kadhalika taarifa hiyo ilieleza kuwa kamati hiyo itaangalia msingi wa hoja (za Millya) na endapo itaridhika, kanuni inaitaka Kamati kuwasilisha hoja hiyo bungeni ili ijadiliwe.
“Kanuni ya 138 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, inamtaka Spika kukalia kiti wakati wa mjadala wa hoja ya kumwondoa Naibu Spika Madarakani,” ilieleza na kuongeza:
“Suala lililowasilishwa na Kinyasi (Millya) kuhusu kusudio la kumwondoa Naibu Spika madarakani, tayari limepokelewa na lipo katika Ofisi ya Spika kwa ajili ya utekelezaji wa masharti ya Kanuni.”
Dk Tulia kutetea Ukawa
Naibu Spika, Dk Tulia Ackson jana alilazimika kuwatetea Ukawa wanaotaka kumng’oa, kwa kuwaeleza wabunge wa CCM kuwa ili kuwakata posho wanaosuasa vikao, kuna haja ya kurekebisha sheria kwa siku zijazo.
Dk Tulia alilazimika kutoa ufafanuzi huo, baada ya wabunge wengi wa CCM kutoa mwongozo wa kutaka wabunge wa Ukawa, waliotangaza kususia vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika wakatwe mshahara na posho.
Alisisitiza kuwa siku zijazo iko haja ya kubadilisha sheria na kanuni zilizopo ili kukabiliana na hali ya namna hiyo, ili kuweka utaratibu mahususi wa kila mbunge kulipwa posho baada ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Dk Tulia akitoa majibu ya miongozo iliyoombwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harison Mwakyembe na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy ambao walitaka kuelezwa kwa nini wabunge hao wamekuwa wakiingia na kutoka na kutaka wakatwe posho na mishahara yao.
Miongozo hiyo iliombwa na wabunge hao wiki iliyopita kutokana na azimio la wabunge wote wa upinzani kususia vikao vyote vinavyoongozwa na Dk Tulia kwa maelezo kuwa hawana imani naye kwa kuwa anaminya demokrasia.
Akijibu miongozo hiyo jana, Dk Tulia alisema Dk Mwakyembe na Kessy walihoji kuhusu wabunge wa upinzani kuingia Bunge la Bajeti, wakisaini na kutoka huku wakilipwa posho na mishahara.
“Wakati akiomba mwongozo wa Spika mheshimiwa Kessy alieleza kwamba kitendo cha wabunge wa upinzani kuingia ukumbini kuweka saini na kuondoka, ilihali wanalipwa posho na mishahara ni sawa na utumishi hewa,”alisema Dk Tulia.
Dk Tulia alisema kuwa Dk Mwakyembe katika kujenga hoja yake alinukuu Ibara ya 26(1) na(2) ya Katiba, vile vile alinukuu Ibara ya 23(1) ya Katiba inayozungumzia ujira kutokana na kazi zao.
“Kutokana na Ibara hizo za Katiba mheshimiwa Harrison Mwakyembe aliomba mwongozo wa Spika kama ni sahihi kwa wabunge wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa nia ya kuweka saini na kuondoka kwenda kupumzika, huku wakiwaacha wabunge wengine wakifanya kazi kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi,” alisema na kuongeza:
“Aliuliza kama wabunge hawa wanastahili kulipwa posho na mishahara kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 23 ya Katiba.”
Dk Tulia alisema kutokana na uamuzi uliowahi kutolewa na Bunge Aprili 27, 2016 kuhusu muongozo wa Spika uliofanana na ulioombwa na wabunge hao wawili ambao uliombwa na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe aliyeuliza kuhusu usahihi wa wabunge wa upinzani kulipwa posho na mishahara wakati hawashiriki kutekeleza wajibu wao wa kuchangia kwenye mjadala wa Bunge la Bajeti.
Alisema katika kujibu mwongozo wa Bashe kiti kilinukuu Ibara ya 73 ya Katiba ambayo inasema, “Wabunge wote wa aina zote watashika madaraka yao kwa mujibu wa Katiba hii, na watalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.”
Dk Tulia akiendelea kunukuu uamuzi huo alisema kuwa kutokana na masharti ya Bunge, mbunge anastahili kulipwa mshahara kila mwezi na anapohudhuria vikao vya Bunge na kamati zake atalipwa posho za vikao kwa kiwango kitakachowekwa na Serikali kwa kuzingatia sheria ya fedha za umma na kanuni zake na masharti ya kanuni za Bunge kuhusu vikao.
“Malipo ya mshahara kwa mbunge ni suala la kikatiba na sheria. Malipo hayo hulipwa kwa mbunge kutokana na nafasi yake ya mbunge kama ilivyotajwa katika Ibara 73 ya Katiba,”alisema Dk Tulia akinukuu uamuzi huo.
Alisema malipo ya posho kwa mbunge yameanzishwa kwa mujibu wa Katiba na kuwekwa katika sheria ya uendeshaji Bunge, sura ya 115 chini ya kifungu cha 19.
Dk Tulia alisema kwa kuwa mbunge anatakiwa kulipwa mshahara kutokana na kuhudhuria vikao na kwa kuwa ni mwakilishi wa wananchi katika kuisimamia Serikali, kutokuhudhuria bungeni na kususia kutoa mchango wake wa mawazo ni kushindwa kutimiza wajibu wake wa kibunge.
Post a Comment