politics

NAOMBA NIPUMZISHWE UWAZIRI ILI NIMSHUHULIKIE LOWASSA



WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema yuko tayari kuuachia uwaziri ili aweze kulithibitishia Bunge kuwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa alihusika katika kashfa ya Richmond.

Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo jana bungeni baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari na Mbunge wa Ubunge Ubungo (Chadema) Said Kubenea kumtuhumu juzi kuwa hakutenda haki mwaka 2008 wakati alipoongoza Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kampuni tata ya ufuaji umeme ya Richmond bila kumhoji Lowassa ambaye alituhumiwa.

Nassari juzi wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alisema Dk. Mwakyembe ameikataa ripoti iliyomchunguza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds kwa madai kuwa haikumhoji mkuu huyo wa mkoa ili hali yeye aliendesha Kamati ya Teule ya Bunge ya Richimond na kumuondoa madarakani Lowassa, licha ya kutokumhoji.

Akijibu tuhuma hizo, Dk. Mwakyembe alisema ni kazi ngumu kwa sasa kumsafisha Lowassa kuhusu tuhuma zilizokuwa zinamkabili kuhusu Richmond.

“Naomba nimalizie kwamba, mimi naahidi, siku ambayo kuna mmoja atakuwa jasiri wa kusema analeta suala la Richmond hapa, mimi naahidi nitamuomba mheshimiwa Rais (John Magufuli) anipumzishe uwaziri, ili niweze kuishughulikia hiyo kesi kiukamilifu iishe moja kwa moja,” alisema Dk. Mwakyembe.

Alisema kamati teule iliyoundwa na Bunge la Tisa kazi yake ilikuwa kuchunguza siyo kutoa maamuzi.

Alisema unapochunguza, suala la kusikiliza siyo lazima na ndiyo maana kamati ilikuja bungeni na kuiwasilisha ripoti ikiwa na mashahidi zaidi ya 40 "wakitusubiri nje.

    “Aliyetakiwa kuhojiwa bungeni akajiuzulu, unamlaumu Mwakyembe kwa hilo, naomba msipotoshe umma kuwa hakuhojiwa, ahojiwe vipi?

    "Unajua ni aibu, ni sawa na mtu anaenda mahakamani anasema unajua polisi hawakunipa haki ya kuhojiwa.


    “Polisi? Uko mahakamani... ndiyo pa kuhojiwa hapo, kwa hiyo ndugu zangu mimi naomba tusipotoshe umma, sisi tulikuwa tumepata nyaraka za serikali 104, na tukahoji watu 75, tuliwauliza maswali 2,717 iko kwenye hansard.”


Alisema Kamati haikuona sababu yoyote ya kumuhoji Lowassa kwa kuwa ilikuwa na ushahidi wote.

    “Mimi niombe, mheshimiwa mwenyekiti (Andrew Chenge) kama kuna mtu yeyote hapa, bado anakereketwa na kesi ya Richmond, aache maneno maneno hapa, leta hiyo kesi hapa kama hatujawanyoa nywele kwa kipande cha chupa.”


Wakati Dk. Mwakyembe akizungumza hayo, Kubenea aliomba utaratibu kwa Mwenyekiti akidai Dk. Mwakyembe analiongopea bunge.

Kubenea alisema Dk. Mwakyembe akiwa mwenyekiti wa kamati hiyo alieleza kuwa mtu anaweza kujiuzulu kwa mambo mawili, moja kwa kuwa yeye mwenyewe anahusika au mbili kwa kuwajibika kwa mambo yaliyofanywa na walio chini yake.

Alisema Kwa mujibu wa ‘hansard’ (kumbukumbu rasmi za bunge), Dk. Mwakyembe alisema Lowassa alijiuzulu kwa mambo yaliyofanywa na walio chini yake lakini leo anasema ana ushahidi wa asilimia 100 kwamba Lowassa alihusika na jambo hilo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kwa idhini yako unipe muda niwasilishe hansard hapa kwenye bunge hili kuthibitisha maneno ya Dk. Mwakyembe ya mwezi Februari mwaka 2008,” alisema Kubenea.

Mara baada ya Kubenea kueleza hayo, Dk. Mwakyembe alisema upinzani hawawezi kumsafisha Lowassa kama madoa ya lami kwa kutumia kamba ya katani au maji, bali warudishe bungeni suala hilo.

Dk. Mwakyembe alimwomba Kubenea kuleta hoja ya Richmond bungeni.

    “Ileteni hapa, naomba kwa Mungu mkiileta hapa nitafurahi kwasababu mimi ninachosema hapa na ushahidi nilionao hapa... sisi tulimkuta huyu jamaa amehusika.


    "Tupo hapa kuthibitisha hilo suala naomba sana kwa sababu mmekuwa na makubaliano ya kumsafisha, hamtaweza kumsafisha. Leteni kesi hapa.”


MAWAZIRI WAOGA
Dk. Mwakyembe pia alijibu hoja iliyotolewa juzi na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa kuwa mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano ni waoga katika kumshauri Rais Magufuli.

Dk. Mwakyembe alisema hoja hiyo haina ukweli wowote na kwamba mawaziri wa serikali ya awamu ya tano wanafanya kazi bila wasiwasi.

    “Ohoo Mawaziri ni waoga, hawana ujasiri, mimi nimekuwa najiuliza ni ujasiri wa aina gani? wa kumkaidi Waziri Mkuu, wa kumkaidi Rais, ujasiri upi?" Aliuliza.


    “Umeona wapi ambapo mawaziri hawaongozwi na kanuni, ya kuwajibika kwa pamoja bungeni katika mfumo wa bunge?"