VITA vya maneno vimezidi kushika kasi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) na sasa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ameibuka na kumtaka aliyekuwa mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, amwache kwa kuwa hana uwezo wa kumfukuza kazi.
Kadhalika, amesema kama kweli Profesa Lipumba anadhani yeye ni mwenyekiti halali, afike makao makuu ya CUF kisiwani Unguja ili kufanya kazi badala ya kukubali aendelee kutumika.
Hivi karibuni Profesa Lipumba alitangaza kumfukuza kazi, Maalim Seif na kumteua Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania bara, Magdalena Sakaya, kuwa kaimu Katibu Mkuu.
Akizungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho katika kisiwa kidogo cha Tumbatu Mvuvini, Maalim Seif alisema anamshangaa Profesa Lipumba kwa madai kwamba yeye ameshindwa kazi kwa kuwa haendi kazini katika ofisi za chama zilikozo Buguruni, Dar es Salaam.
"Eti nimeshindwa kazi akidai kuwa siendi ofisi kuu ya CUF Buguruni. Mbona yeye haji makao makuu ya CUF Mtendeni. Lipumba hana mamlaka ya kuniondoa nafasi yangu ya ukatibu mkuu,” alisema.
Alisema tangu Agosti, 2015, Lipumba hajawahi kukanyaga makao makuu ya CUF Mtendeni na kwamba hata kama angekuwa Mwenyekiti halali wa chama, alipaswa kumwita na kumhoji kwa nini haendi ofisi kuu za chama Buguruni kuliko kuchukua madaraka ya kutangaza kuwa amemtimua.
Maalim Seif pia alikemea siasa za chuki na uhasama zilizotawala kisiwani humo kati ya CCM na CUF na kusema zimesababisha mapigano na hujuma ikiwamo kuchomeana nyumba kutokana na itikadi za vyama.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema Profesa Lipumba ametumika na amefanya kazi kubwa ya kukihujumu chama huku akiungwa mkono na baadhi ya wanachama.
Mazrui pia alimwomba Rais John Magufuli kumtimua Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa madai kuwa ni miongoni mwa watendaji wabovu wa serikali.
Alisema utendaji mbovu wa Jaji Mutungi umesababisha mtafaruku mkubwa na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF.
“Rais Magufuli anatumbua watendaji ambao si waadilifu, lakini Msajili amemwacha kwani anapaswa kutumbuliwa kwa sababu ameivuruga nchi,” alisema.
Alisema Msajili huyo amempa uhalali Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF, wakati alijiuzulu kabla ya uchaguzi mkuu na sasa amekuwa akikihujumu chama.
SHOW YA MSAMI BABY KWENYE FM BEACH PARTY MKOANI TANGA ITAZAME HAPA