IJUMAA nyingine ninapokukaribisha msomaji wangu katika ukurasa wetu huu, tujadiliane na kuzungumza mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.
Leo nataka kuzungumza zaidi na ndugu zetu wa upande wa pili kuhusu sifa za mume au mwanaume bora. Wanaume wanaweza kudhani mada hii haiwahusu lakini inawagusa sana kwa sababu wao ndiyo wanaozungumziwa kwa hiyo ni vizuri wakaelewa sifa wanazopaswa kuwa nazo.
Wanawake wengi ni wepesi sana wa kudanganyika na sifa za nje za mwanaume.Ukipata nafasi ya kuwasikiliza wanawake juu ya wanaume wanaowapenda, utashangaa kusikia wakisema kwamba mwanaume bora ni yule mwenye gari la kifahari, mwenye nyumba, mwenye fedha au mwenye mwili wenye misuli iliyojengeka vizuri au anayepiga pamba kali.
Wengi wanashindwa kuelewa kwamba sifa hizo za nje hazitoshi kutoa tathmini ya mwanaume bora na matokeo yake, wanajikuta wakiingizwa kwenye mitego ya wanaume kwa urahisi. Kwa kuwa wanaume wanajua wanawake wanapenda nini, siku hizi kuna mtindo mpya wa namna ya kuwanasa wanawake.
Mwanaume yupo tayari kwenda kuazima gari kwa rafiki yake au kukodisha, yupo tayari kwenda kuazima nguo kwa rafiki zake na kwenda kuingia madeni kwa kukopa fedha ili aonekane anazo. Wanaume wanalazimika kudanganya uhalisia wa maisha yao ili waweze kutimiza haja zao kwa wanawake.
Wengine wanashindwa kujishughulisha katika kazi zinazoweza kuyabadilisha maisha yao na badala yake wanashinda Gym kutanua vifua ili wawanase wasichana warembo! Kama ilivyokuwa kwa sifa na vigezo vya mwanamke bora, kwa upande wa wanaume pia ni hivyohivyo. Sifa za nje pekee hazitoshi kumfanya mtu amjue mwanaume bora ni yupi.
Hujawahi kukutana na mwanamke mwenye sifa zote zinazotakiwa akiwa amenasa kwenye penzi la mwanaume ambaye jamii nzima inajiuliza ‘amempendea nini yule? Mbona hawafanani?’
Hujawahi kuona kwamba mwanamke anawakataa wanaume wenye fedha, magari na kila kitu lakini anamng’ang’ania mwanaume ambaye jamii inamtafsiri kwamba hana sifa wala vigezo vya kuitwa mume au baba bora? Mwonekano wa nje, fedha, magari, majumba na vitu vingine kama hivyo havina maana kama mhusika anakosa sifa za ndani ambazo ndizo hasa zinazomfanya mwanaume awe mume bora au baba bora.
Hujawahi kuona wanandoa ambao walioana kwa ndoa za kifahari, wakaishi maisha ya duniani kama wapo peponi kutokana na utajiri mkubwa walionao, mwisho wakaachana na kupeana talaka kwa vurugu kubwa? Hujawahi kusikia wanawake ambao licha ya waume zao kuwa na kila kitu, zikiwemo fedha nyingi, magari ya kifahari na majumba ya maana wanazikimbia ndoa zao na kwenda kuolewa na walala hoi? Mifano hiyo inatosha kukufanya ujiongeze kwamba kumbe ubora wa mume au mwanaume, ni zaidi ya vile ambavyo watu wengi wanaamini.
Kwa kuwa mimi si mjuzi wa kila kitu, huwa napenda zaidi kusikia kutoka kwako msomaji wangu. Hebu niambie, kama sifa hizo za nje siyo zinazoweza kutoa tathmini ya ubora wa mume, kumbe mwanaume au mume bora anapaswa kuwa na sifa na vigezo vipi?
SHOW YA MSAMI BABY KWENYE FM BEACH PARTY MKOANI TANGA ITAZAME HAPA