Raia takriban 90 wa Somalia na wawili wa Kenya wametimuliwa kutoka Marekani saa chache baada ya taarifa kuibuka kwamba Rais Donald Trump atakabiliana na watu wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.
Wote wamewasili katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Msemaji wa serikali ya Kenya Eric Kiraithe ameambia BBC kwamba raia hao wa Somalia watasafirishwa moja kwa moja hadi Mogadishu.
“Ni watu 90 kulingana na habari ambazo tulipewa. Wakati unaondolewa nchi fulani kurejeshwa kwenu, huwa unarejeshwa hadi kwenu,” ameambia BBC.
Kuhusu sababu iliyowafanya kufurushwa, Bw Kiraithe amesema: “Inategemea sheria za nchi ambayo walikuwa wamehamia (Marekani),”
Anatarajiwa kuweka masharti makali kwa raia wa mataifa saba ya Mashariki ya Kati na Afrika yenye idadi kubwa ya Waislamu wanaotafuta viza za kwenda Marekani.
Wakati wa kampeni yake ya urais, Donald Trump aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.