exclusive
Exclusive: P-Funk aishtaki Walt Disney kwa kutumia wimbo wake kwenye ‘Queen of Katwe’, Chameleone adaiwa kulipwa na kuchuna
0
Comments
Producer mkongwe, P-Funk Majani wa Bongo Records ameishtaki kampuni maarufu ya filamu nchini Marekani, Walt Disney, kwa kutumia wimbo Bomboclat wa Jose Chameleone na Weasel kwenye soundtrack ya filamu yake Queen of Katwe (2016) iliyochezwa na mshindi wa tuzo za Oscar, Lupita Nyong’o.
Beat ya wimbo huo ilitayarishwa na P-Funk na ilitumika awali kwenye wimbo wa Professor Jay, Nikusaidiaje, lakini haki miliki za kazi hiyo zipo chini ya label yake, Bongo Records.
Awali, baada ya Majani kubaini kuwa wimbo huo umetumika kwenye filamu hiyo bila kupewa taarifa, alimtafuta Chameleone ili kumuuliza kwanini hakumhusisha kwenye makubaliano ya kutumika kwa kazi hiyo.
“Ningependa kupata updates kuhusu matumizi ya kazi yangu kwenye soundtrack ya movie mpya ya Disney. Tena, umepiga move ya kibabylon,” Majani alimuambia Chameleone kwenye DM ya mtandao wa Instagram.
“Ndio kaka, siwezi kuDM chochote, na sina namba yako ya WhatsApp,” Chameleone alijibu.
Majani alimpa namba yake ya simu na kuongeza, “Nahitaji sana kujua kwanini sikuhusishwa kwenye makubaliano yako kuhusiana na Bomboclat kuwekwa kwenye soundrack. Unajua kuwa hiyo ni mali bunifu yangu. Kama ninavyokumbuka, haukuwahi kumalizia malipo na neno lako lilikuwa “Bro tulitumia tu kama riddim si kwa kuuza ama kitu kama hicho” nini kimetokea? Miaka 10 baadaye, umekiuka haki miliki yangu kama mtunzi wa wimbo huo na pia haki zangu za utambuzi kwa kutonipa credit kwa kazi yangu,”aliandika Majani kwenye mazungumzo hayo ambayo Bongo5 imeyapata.
Chameleone alijibu,” Ah bro haikuwa hivyo, unaweza kunitumia namba yako ya simu kwaajili ya maelezo sababu inabidi tuliweke hili sawa. Sikukiuka haki zako ama kitu chochote nahitaji tu kueleza kwa ufupi. Nimejaribu kukutafuta Dar lakini muda hakukubali. Nitawezaje kukupigia sababu utaelewa.”
“Majani, nimejaribu kukusaka kaka, nimepiga siku nzima,” aliendelea Chameleone.
“Nilitoa credit na nilipata nyaraka zote kuhusiana na matumizi ya wimbo. Nisamehe kama unajisikia hivyo, lakini kiukweli nilikubali matumizi ya Bomboclat sababu niliona kama ni fursa kubwa ya kufahamika. Malipo yalikuwa madafu ambayo hata bado hayajatolewa. Nilipata cheki hata sasa ni kama $2,000,” msanii huyo maarufu wa Uganda alijitetea.
Utetezi wote huo wa Chameleone haukumgusa Majani. Mtayarishaji huyo mkongwe wa muziki aliamua kufuata mchakato unaotakiwa kudai haki yake kwa kupeleka suala lake COSOTA ambao nao waliandika barua kwa chama cha haki miliki nchini Uganda (UPRS), Disemba 7 mwaka 2016. Barua hiyo bado haijajibiwa hadi sasa.
“Hata hawajajibu [UPRS], they just kept quiet, wanaipuuzia,” Majani ameiambia Bongo5.
“Hata hawajajibu [UPRS], they just kept quiet, wanaipuuzia,” Majani ameiambia Bongo5.
“Sasa tulichokifanya, imebidi twende kwa Walt Disney, kwasababu hatukupata jibu kutoka Uganda. Kwahiyo sasa tunaishtaki Walt Disney, Walt Disney wamekubali tuyamalize nje ya mahakama lakini pia watashughulika na Chameleone,” anasema Majani.
“Niwe na wasiwasi, nijali? Hakuna, kwasababu [Chalemeone] hakunijali mara ya kwanza. Huo ulikuwa ni muziki wangu niliotengeneza chini ya label yangu, alichukua instrumental, kaiba akaamua kuimbia akatuletea longo longo. Hiyo dola 2,000 alitakiwa alipe kipindi kile, tulikubaliana hivyo akaponyoka hajatoa hela, alizuga tu,” amesisitiza Majani.
Kwa upande mwingine P-Funk amedai kuwa Disney hawajamlipa $2,000 Chameleone kama anavyodai na kwamba wanaweza kuwa walimlipa $50,000. “Unakuta muda wote unabeba ule uchungu,” anasema mtayarishaji huyo.
“Unaacha shughuli zako zingine unaanza kufuatilia, uende COSOTA ukafuatilie hilo suala mara umpigie wakili wa Marekani awasiliane na Walt Disney hela inakutoka, wakili wa Marekani anataka $400 kwa saa, anataka retainer fee ya $2,000, all these, just for this, why?”
Queen of Katwe ilizinduliwa Septemba 23 na ilitumia bajeti ya dola milioni 15 kuikamilisha. Soundtrack ya filamu hiyo inajumuisha pia nyimbo za wasanii wengine kama Alicia Keys, Davido, Eddy Kenzo, Radio and Weasel, Michael Kiwanuka, Bobi Wine na wengine.