hot news

Nape, Zitto wavaana muswada wa habari-1

Baada ya kupambana na mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, vita kuhusu Muswada wa Huduma za Habari umehamia nje ya chombo hicho, safari hii Zitto Kabwe akipambana na Wazari ya Habari, Nape Nnauye.

Vita baina ya wawili hao inafanyika kwenye mitandao ya kijamii ambako Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, ametoa maoni yake kuhusu muswada huo na baadaye Nape kumjibu kabla ya Zitto kumjibu tena.

Zitto, ambaye aling’ara alipoingia bungeni akiwa kijana mdogo na kuchachafya chombo hicho kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja, alipambana vikali na Peter Serukamba wakati muswada huo uliposomwa kwenye kamati hiyo mapema wiki hii.
Hoja ya Zitto ilianzia katika kutaka kujua ni kiasi gani wadau wa habari wameshirikishwa katika kuupitia muswada huo, huku Serukamba, ambaye ni mwenyekiti wa kamati akitoa ufafanuzi.

Vita ya Zitto na Nape

Zitto, ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, alitoa waraka kwenye mitandao ya jamii akiuponda muswada huo kwa kuuita kuwa ni“hatari”.

Hoja za Zitto
Serikali ya Awamu ya Tano imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria kutunga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari. Muswada wa Sheria hiyo sasa upo mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuchambuliwa na kisha kuwasilishwa bungeni. Kwa mujibu wa kifungu cha 84 cha Kanuni za Bunge, 84 Kamati ya Bunge inawajibika kuutangaza muswada na kupokea maoni ya wadau mbalimbali.
 
Kwa hakika wadau wa muswada huu ni wananchi wote kwani haki ya kupata habari ni haki ya kikatiba. Hata hivyo, waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari na mitambo ya kuchapisha magazeti na majarida ni makundi yatakayoathirika moja kwa moja na muswada huu utakapokuwa sheria.

Hata hivyo, muswada unapelekwa mbio na mwenyekiti wa kamati katishia kuwa iwapo wadau hawatatoa maoni, kamati yake itaendelea na kazi zake za kutunga sheria.

Kwa muda mrefu sana, waandishi wa habari na wanazuoni mbalimbali wamekuwa wakitaka kuwepo na sheria ya kusimamia tasnia ya habari. 

Ninaambiwa kuwa juhudi za kutunga sheria hii ni mchakato wa zaidi ya miaka 20, tangu mwaka 1993 na muswada wa kusajili waandishi wa habari uliondolewa bungeni baada ya kuwasilishwa na Dk William Shija wakati ule akiwa Waziri wa Wizara ya Habari na Utangazaji, ambaye sasa ni marehemu.

Vile vile kumekuwa na kilio kikubwa cha vyombo vya habari kufungiwa kwa kutumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo inampa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari. 

Wananchi wengi na wapenda demokrasia walitarajia kwamba sheria mpya ingeweza kuondoa sheria kandamizi na kuweka uhuru wa vyombo vya habari ipasavyo. Hicho sicho kilicholetwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli.

Muswada uliopo mbele ya kamati ya Bunge unatoa tafsiri pana sana ya vyombo vya habari. Sehemu ya 3 ya muswada inatamka chombo cha habari ni pamoja na gazeti, kituo cha redio na televisheni, ikiwemo mitandao ya kijamii (online platforms). Muswada unatamka kuwa ni lazima media house (chombo vya habari) iwe na leseni maalumu kwa ajili kufanya kazi na waandishi wa chombo hicho ni lazima waandikishwe kwenye chombo kiitwacho Accreditation Board (Bodi ya Ithibati).

 Iwapo sheria hii itatungwa, maana yake ni kwamba mtandao kama wa jamiiforums utapaswa kuandikishwa na watu wote wanaotoa maoni yao kwenye mtandao huo lazima wawe na ithibati! Haitaishia hapo, bali hata blogs nk zitapaswa kuandikishwa kama ilivyo magazeti. Hatua hii itaminya sana uhuru wa watu kupata habari na kupashana habari. Hata uhuru wa kujieleza utaminywa sana kupitia mitandao ya kijamii.

Muswada unataka kuwepo na sheria ya Serikali kuamua vyombo vya habari viandike nini na vitangaze nini. Sehemu ya 7(1)(b)(iv) inatamka wazi kwamba Waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari fulani au masuala fulani yenye umuhimu kwa Taifa. Itakumbukwa kwamba muswada uliopita ambao ulikataliwa ulitaka ifikapo saa 2:00 usiku televisheni na redio zote ziungane na TBC kutangaza taarifa ya habari.

Kifungu hiki ndio kitatumika kufanya suala hilo kwa amri ya waziri. Kifungu hiki pia kinampa Waziri wa Habari mamlaka ya kuelekeza chombo cha habari kutotoa habari fulani kwa utashi wa waziri. Ni dhahiri kuwa huu ni ukiukwaji mkubwa sana wa uhuru wa habari na kuwa kikwazo kikubwa kwa kazi za waandishi. Kwa kutumia kifungu hiki, Waziri wa Habari anaweza kuagiza magazeti yote yasiandike habari za IPTL Tegeta Escrow na waziri atakuwa ndani ya sheria.

Muswada pia unampa Waziri wa Habari mamlaka ya kutoa Masharti ya Kazi za Vyombo vya Habari (Terms and Conditions ). Hii inatia nguvu kifungu hicho hapo juu kuhusu maelekezo ya habari za kutolewa na kutotolewa na vyombo vya habari.

Muswada huu umerudisha vifungu vyote kandamizi vilivyopo kwenye sheria ya magazeti ya mwaka 1976. 

Kwa mfano kifungu cha 54-56 kinampa Waziri haki ya kutamka kwamba gazeti fulani au kitabu fulani kisisambazwe nchini au kuzalishwa nchini. Kwenye masuala mengine, Mkurugenzi wa Habari Maelezo na Jeshi la Polisi linaweza kuingia kwa nguvu na kuchukua mitambo inayozalisha magazeti kwa sababu tu gazeti hilo limechapisha habari ambayo kwa maoni ya Serikali ni habari za kichochezi.

Muswada umetafsiri uchochezi kuwa ni pamoja na kuandika au kutangaza mambo ambayo yanaweza kutafsiriwa kuwa yanaleta chuki ya wananchi dhidi ya Serikali. Kwa kutumia kifungu hiki, mbunge wa upinzani akihutubia na kuonyesha ufisadi serikalini, sheria hii inaweza kutumika kufuta vyombo vya habari vilivyoandika au kutangaza habari hiyo.

Kwa ufupi, huu ni muswada mbaya kuliko sheria ya magazeti ya sasa. Huu muswada unairudisha nchi nyuma katika juhudi za kujenga Taifa lenye Haki na wajibu. Ni sheria kandamizi ambazo kama Jaji Francis Nyalali angekuwa hai, angeijumuisha katika sheria 40 kandamizi. Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujenga Taifa lenye giza. Rais Magufuli ameamua kukataa katakata kuhojiwa na kukosolewa kwa kuhakikisha kuwa anavibana vyombo vya habari nchini.

Nilipata kusema huko nyuma kwamba, Serikali ikishamaliza kuvibana vyama vya upinzani itavibana vyombo vya habari. Utabiri ule umetimia kupitia Sheria ya Huduma za Habari inayoelekea kutungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dodoma, 20/10/2016
Nape amjibu
Naziona juhudi kubwa za Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kujaribu kupotosha jamii kwa kutosema ukweli kuhusu masuala kadhaa yahusuyo Muswada wa Huduma za Habari, 2016.
Kwa kawaida mimi huwa si mtu wa kujibu hoja zinazotolewa kinafiki na kioga kama alivyofanya rafiki yangu Zitto Zuberi Kabwe. Kwa hali ya kawaida ningeweza kumpuuza kabisa, lakini kwa hili uvumilivu wangu kwa kiwango hiki cha unafiki umefikia ukingoni. Hivyo nitalazimika kujibu baadhi ya hoja.

Nimesoma kwa masikitiko sana sana, makala ndefu kidogo aliyoisambaza ndugu yangu na mwanasiasa kijana mwenzangu, Zitto Zuberi Kabwe kuhusu alichodai ni hatari ya Mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari 2016.

Muswada huu uliochapishwa na kuwekwa hadharani tangu Septemba, 2016, pamoja na mambo mengine unakwenda kuhitimisha safari ya zaidi ya miaka 20 ya wadau wa habari nchini kuwa si tu kuwa na sheria nzuri itakayoratibu kazi na kulinda maslahi yao, bali sheria inayoitangaza rasmi kazi hii kuwa taaluma kamili.

Hata hivyo, akiyatumikia maslahi yasiyo wazi kwa sasa, akiongozwa na unafiki wa hali ya juu kabisa kupata kuushuhudia kwake, na baada ya kujaribu kuzuia muswada huu kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii na juhudi zake hizo kushindwa vibaya, mbunge mwenzangu Zitto Kabwe ameanza kupayuka mitandaoni akieneza uzushi na kila aina ya uongo na upotoshaji kuhusu muswada huu.

Inahitaji ujasiri wa kinafiki kuandika aliyoyaandika mwanasiasa mwenzangu kijana Zitto Zuberi Kabwe. Licha ya kuwa nimekuwa nikimheshimu kwa muda mrefu, na bado namheshimu na kumpenda kama kijana mwenzangu, unafiki huu wa kutumikia masilahi binafsi umenistua sana.

Kama nilivyosema nitayajibu baadhi ya madai yake kama ifuatavyo:-
Hoja ya kushirikishwa wadau
Zitto anajaribu kujenga picha kuwa muswada huu haukushirikisha wadau. Ndugu yangu huyu, huku akiwa anajua kuwa katika utungaji wa mswaada kuna hatua mbili za kutoa maoni.

Hatua ya kwanza ni pale Serikali inapokuwa inatengeneza mswaada husika kabla ya kuupeleka kwenye vikao vya kiserikali. Kwa hatua za kuupitisha, wadau HUSHIRIKISHWA ili kutoa maoni yao. Na kwa mswaada wa Huduma za Vyombo vya Habari,2016, wadauwameshirikishwa tena na ushahidi wa maandishi wa ushiriki wao na maoni yao upo.

Hatua ya pili ya utoaji maoni huwa ni baada ya muswada kusomwa mara ya kwanza bungeni, muswada husika hukabidhiwa kwa kamati ya Bunge, na ukishakabidhiwa huwa ni waraka huru kwa umma kuusoma na kutoa maoni yao (public document) kwa Kamati ya Bunge.

Hili pia limefanyika mpaka hatua ya wadau kuitwa na kuja Dodoma na waliomba mbele ya Kamati wapewe muda wakamilishe kazi ya kusoma na kutoa maoni yao. Na Mwenyekiti wa Kamati, Peter Serukamba (Mbunge) kwa uamuzi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wakaamua kuwaongezea muda wadau kwa wiki moja kukamilisha kazi hiyo, shughuli inayoendelea sasa.
Zitto kwa makusudi aliamua kujaribu kuzuia bila mafanikio hatua hii ya pili isifanyike.

Hoja yake hiyo ilianguka mbele ya Kamati tulipoonyesha ushahidi wa wazi na wa nyaraka kuwa wadau wakuu wote si tu walishiriki katika hatua za ndani ya Serikali kutoa maoni na sasa watashiriki zaidi katika hatua hizi za Bunge, bali sehemu kubwa ya maoni yao yaliingizwa katika muswada wa sasa. Zaidi ya asilimia 90 ya maoni ya wadau yamezingatiwa katika muswada huu.

Alipoona kashindwa kabisa akaamua kuondoka Dodoma akasafiri na kusambaza waraka wa kizushi ili kufurahisha waliomtuma badala ya kuchangia kuboresha muswada husika.
Hoja ya kulazimisha vyombo vya Habari kujiunga na TBC
Zitto pia anaeneza uongo kwamba muswada huu unadhamiria kuvifanya vyombo vya habari, hususan TV kulazimishwa kujiunga na TBC kwenye vipindi vyake.

Kwanza nina wasiwasi kama ameusoma muswada huu na kama ameusoma naanza kuamini hana muswada sahihi. Au ndio kaamua kutoa maoni akiongozwa na unafiki.
Hata hivyo, hili tumelifafanua katika kamati. Kwa bahati mbaya hakuhudhuria ili kupata uelewa mpana.

 Mosi, hakuna kifungu kama hicho katika muswada huu; pili, hakuna dhamira hiyo kwenye muswada huu; na tatu, Serikali haina hata wazo hilo.

Mitandao ya kijamii
Zitto, katika kutimiza malengo na maslahi yake, anapotosha kuwa muswada huu unakusudia kuzibana blogs na kutaja mitandao ya kijamii kama jamiiforums kuwa nayo itatakiwa kusajiliwa. Mtu huyu ni wa kumwonea huruma. Bahati mbaya muswada huo hauna mamlaka wala nia hiyo. Kifungu cha 3 cha sheria kiko wazi kuwa usajili utahusu magazeti na majarida na machapisho yao ya mitandaoni (magazeti mtandao ya magazeti hayo rasmi na si mitandao yote au mingine ya kijamii kama anavyopotosha).
Na kwakuwa nakala ya muswada huu ina tafsiri ya Kiingereza na Kiswahili, sitaki kuamini kuwa Zitto hakusoma hili, au waliomtuma hawakusoma vizuri hili.

Itaendelea 👆👆

Zitto anakwenda mbali kudai wachangiaji kama wa jamiiforums watatakiwa wafanyiwe ithibati! Bila shaka mwenzetu huyu anajadili muswada mwingine kabisa.
Muswada huu hauhusu wala hakujapata kuwa na fikra za kudhibiti au kuratibu mitandao ya kijamii na kuwataka watumiaji wa mitandao hiyo eti wasajiliwe. Huu ni upuuzi mwingine wa kupuuzwa.

Ipo hoja ya Waziri kupewa mamlaka kuagiza chombo chochote kutangaza jambo lenye umuhimu kwa umma: Katika hili pia tumsamehe kwa sababu hahudhurii vikao vya kamati wakati wa mijadala hii. Hili limejadiliwa kwa kina na wahusika kuelewana. Hakuna kifungu kinachompa mamlaka hayo Waziri. Bali kifungu kilichopo kinaipa fursa Serikali kuvishauri/kuvielekeza(Govt MAY) vyombo vya habari kuungana pamoja kulinda maslahi ya Taifa kunapokuwa na jambo la muhimu kama vile nchi kuwa VITANI au majanga makubwa.

Zitto kama kijana wa Kitanzania kama haoni umuhimu wa hili, basi hakuna namna nyingine ya kumsaidia.
Kwamba muswada unampa Waziri wa Habari majukumu ya kutoa masharti kwa kazi za vyombo vya habari na kwamba anaweza kuamua gazeti lichapishwe habari aitakayo.

Hili ni eneo jingine linalothibitisha kuwa hapa tunajihusisha na mtu mwenye malengo ya hatari sana na anayejaribu kuweka matazamio yake katika jambo la muhimu kama hili. Muswada huu hauna kifungu hicho zaidi ya Waziri kupewa uwezo wa kisheria, kama ilivyo katika sheria nyingine, kutunga kanuni za kutekeleza sheria hii. Hili nalo Zitto hataki!!!!
Zitto anasema muswada huu unampa mamlaka Waziri kuzuia chapisho au kitabu fulani kisisambazwe nchini.
Ni kweli muswada umetoa mamlaka hayo, lakini Zitto ameamua kutosema ukweli wote.

Muswada unampa Waziri mamlaka hayo si kwa kila jarida au kitabu bali yale tu ambayo yamedhihirika kuchapisha habari huku yakivunja sheria za nchi. Kama Zitto anafikiri nchi yetu itaruhusu majarida yanayotaka kuhamamsisha vita na uvunjifu wa amani nchini, ajue hakuna nchi inayoruhusu mambo hayo.

Zitto anazungumzia kuwepo kwa vifungu vya uchochezi akitoa tafsiri kuwa wabunge wa upinzani watabanwa.

Kwanza katika hili, lazima ijulikane kuwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ukiwemo Mkataba wa Kimataifa Juu ya Haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966, masuala yote yanayohusu kusababisha athari kwa usalama wa taifa ni ukomo unaokubalika wa uhuru wa habari (allowable restriction to press freedom).

Uandishi wa habari kama taaluma nyingine unabeba haki na wajibu. Moja ya masuala ambayo waandishi wanapaswa kubeba wajibu kwayo ni kutosababisha hatari kwa usalama wa Taifa kwa kusababisha vurugu, chuki katika jamii (uchochezi). Hivyo katika kuweka vifungu hivi muswada umezingatia ukweli huo wa sheria za kimataifa.

Hata hivyo ieleweke, tofauti na Zitto anavyopotosha, sheria hii imekwenda mbali zaidi kwa ruhusu wananchi na watu wengine kuikosoa Serikali na utekelezaji wa sera zake.

Sheria inasema haitakabla..
uchochezi kama mtu atatoa maoni yake kwa minajili ya kukosoa makosa katika Serikali, makosa katika utekelezaji wa sera (kifungu cha 49[2]). Huu ni uhuru mkubwa sana kuwahi kutamkwa na sheria.

Mwisho, namshauri Ndugu Zitto Kabwe apunguze kuishi kinafiki. Akasome tena muswada huu na alete hoja zake kwenye Kamati ya Bungeni zijadiliwe. Aache kupotosha umma mitandaoni na aache kujiweka karibu zaidi na vibaraka.

Muswada huu, narudia tena, unakwenda kuifanya sekta ya habari kuwa taaluma inayoheshimika. Ni muswada unaokwenda kuipa heshima taaluma hii na kila mmoja wetu awe tayari kwa mageuzi haya.

Katika kuifanya fani hii kuwa taaluma, tunafahamu kuwa wapo waliozoea mambo ya kale na yale yale na kwamba watapinga. Tunafahamu wapo watakaoona wanahabari waliowaajiri watadai maslahi zaidi na wapo watakaoona fani hii kuwa taaluma kamili watashindwa kuitumia kwa maslahi yao. Wanahabari na wananchi tuungane kuwakataa wenye maslahi binafsi katika hili.

Tuungane kutoa maoni ili tuwe na muswada bora zaidi na utakaoifanya sekta ya habari kuwa na mchango mzuri zaidi kwa nchi yetu.

Kwasasa niishie hapa , lakini nitaendelea na awamu ya pili hata ya tatu ya ufafanuzi ikibidi. Uzalendo katika hili utashinda unafiki na utumwa wa kubeba mawazo ya watwana wachache walizoea vya kunyonga ambavyo kuchinja kwao msamiati!
Majibu ya Zitto
Majibu yangu Kwa HOJA za Nape Nnauye kuhusu muswada wa Huduma za habari, 2016
Ndugu yangu Nape Nnauye amejibu andiko langu nililolitoa jana kuhusu muswada tajwa. Kama ilivyo ada ya siasa za kijingajinga, Nape amejibu andiko langu Kwa kunishambulia binafsi na kuweka Hoja zake mbalimbali. Mimi sitamjibu Nape namna yake maana wenye busara wametufunza ‘ when they go low go high ‘. Nitajibu Hoja za Nape na sitamjibu Nape. Hata kwenye andiko langu sikutamka neno Nape Nnauye kwani Siasa zangu sio Siasa za mtu bali za masuala. Sitahangaika na mtu bali hoja ili kujenga.

Hoja ya Kushirikishwa wadau
Kanuni za Bunge (kanuni ya 84 ) zinataka kwamba Muswada ukishasomwa kwa mara ya kwanza, Bunge lifanye MATANGAZO Kwa umma ili kuhakikisha kuwa umma unaelewa maudhui ya muswada na kuwezesha wananchi kutoa maoni yao. Kwanza, kwa muswada huu Bunge halikutoa matangazo yeyote (kwa taarifa tu ni kwamba hata Kamati ya Bunge ilishindwa kutoa photocopy nakala za uchambuzi wa muswada kutoka kwa wanasheria wa Bunge Kwa sababu Bunge halina Fedha. Bunge halina Fedha kutoa photocopy ya nyaraka za wabunge kufanyia Kazi ).

Wadau wote waliokuja mbele ya Kamati ya Bunge walitamka dhahiri kwamba wamepewa taarifa ya kutokea mbele ya Kamati Siku 2 kabla ya vikao na hivyo wameomba muda zaidi wa kutoa maoni yao. Labda mi kutokana na uchanga wa shughuli za Bunge, Waziri anajenga hoja kwamba ushiriki ulianzia kabla
Mtu yeyote anayejua namna Bunge linafanya kazi, atakwambia muswada ni muswada pale ambapo umechapishwa kwenye Gazeti la Serikali na kusomwa mara ya kwanza Bungeni. Wadau wote waliiambia kamati kwamba Kwa muswada huu ndio walikuwa wanashirikishwa kwa mara ya kwanza pale mbele ya Kamati. Hivyo wadau hawakushirikishwa kwenye muswada huu tangu umesomwa kwa mara ya kwanza Bungeni.

Kama Serikali ina ushahidi wowote ule kwamba kati ya Septemba na sasa muswada huu umehusisha mdau yeyote, waweke wazi uthibitisho huo. Nyaraka zinazoonyeshwa na Serikali ni za miaka ya nyuma kabla ya muswada kuwa muswada. Ushirikishaji unaanza rasmi pale muswada upo gazetted na umesomwa bungeni.

Hoja ya kulazimisha vyombo vya Habari nchini kujiunga na TBC
Majibu ya Hoja
Itakumbukwa kuwa muswada wa awali ulikuwa na kifungu hiki na wadau wakapiga kelele sana kukataa. Ukisoma muswada huu kwa juu juu, utaweza kuona kuwa kifungu hiki hakipo. Mtu mwenye dhamira ovu huficha huficha mambo yake. Kwenye muswada huu mambo mengi yaliyokataliwa Na wadau sasa yamewekwa kiujanja kwa kuweka mamlaka hayo Kwa Waziri mwenye dhamana ya habari. Serikali inaposema hakuna kifungu hicho, haisemi kuna kifungu gani. Nitawaeleza kifungu kilichowekwa ambacho ndicho kitatumika na Waziri kufanya haya bila kuhojiwa Na mtu yeyote yule, kupitia kanuni.

Sehemu ya 7(1)(b)(iv) inatamka wazi kwamba Waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari fulani au masuala fulani yenye umuhimu kwa Taifa.

Serikali itatumia kifungu hiki kutekeleza jambo lile lile ambalo wadau walikataa kuwekwa sheria siku za nyuma. Serikali italiweka lwa mlango wa nyuma. Mbaya zaidi muswada unatamka wazi kwamba waziri mwenye dhamana ataweka TERMS and CONDITIONS kwa uendeshaji wa ‘media houses’. Hivyo Hata wakifuta kifungu hicho cha 7, bado Waziri kapewa mamlaka makubwa sana ya kuamua chombo cha habari kinaendeshwaje. Ni dhahiri kwamba Waziri ama anajua haya au kawekewa vifungu ambavyo yeye binafsi hajui tafsiri zake, lakini atashangazwa katika utekelezaji wa sheria. Kifungu cha 60(2)(a) (Minister to make regulations for TERMS and CONDITIONS for OPERATIONS of licensed media house) inampa mamlaka hayo Waziri kiasi ambacho ataweza kuendesha vyombo vya habari atakavyo yeye. Muswada huu unamfanya Waziri wa Habari kuwa Mhariri Mkuu wa Taifa.

Mitandao ya kijamii:
Muswada uliopo mbele ya Kamati ya Bunge unatoa tafsiri pana sana ya vyombo vya habari. Sehemu ya 3 ya muswada inatamka chombo cha habari ni pamoja na gazeti, kituo cha radio na televisheni ikiwemo mitandao ya kijamii (online platforms).

Napenda umma wa Watanzania ufahamu kwamba muswada ni wa Kiingereza. Muswada wa Kiswahili ni kwa ajili tu ya kuwezesha wabunge wasiojua Kiingereza kuweza kuelewa vifungu vya muswada. Muswada ni wa Kiingereza, ndio rasmi. Mahakamani hawatatumia muswada wa Kiswahili, bali muswada rasmi.

Tafsiri ya online platforms haikuwekwa kwenye muswada. Tafsiri ya media ndio imeweka hilo la online platforms. Naomba mtu yeyote aende Google Na kuandika online platform atapata tafsiri ni nini. Nitasaidia kidogo hapa.

“Social media is defined as ‘online interactions among people in which they create, share, and exchange information and ideas in virtual communities, networks and their associated platform’”. Serikali itatumia tafsiri hii ya kwenye muswada kubana mitandao ya kijamii. Hivi Watanzania mmesahau kesi ambazo wananchi wanapewa kupitia sheria ya Cyber Crime? Hivi mnasahau kuwa Rais alisema anatamani mitandao ya kijamii malaika washuke waizime? Malaika watashuka kwa kupitia muswada huu. Muswada huu una nia ovu kabisa ya kukandamiza uhuru wa habari.

Itaendelea
Post a Comment

Post a Comment