MAKALA

28.8% ya watoto wanatumikishwa nchini Tanzania



Takwimu zinaonesha kuwa watoto milioni 4.3 wanatumikishwa katika kazi za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na madini nchini Tanzania kati ya watoto milioni 15 hali inayochangiwa na kipato duni katika ngazi ya kaya.

Hayo yamebainika leo jijini Dar es salaam, wakati serikali ya Tanzania, ikizindua Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto ya Mwaka 2014.

Katika Ripoti hiyo yenye Kurasa Ishirini na Mbili, imefanyika katika mikoa ya Tanzania Bara na kubaini kuwa asilimia 28.8 ya watoto milioni 4.2 wanatumikishwa katika shughuli mbalimbali ambapo kati yao asilimia 92 wanafanya kazi katika mazingira hatarishi na kupewa ujira mdogo wa kati ya shilingi 5000 na 6000 kwa mwezi.

Akizungumza kabla ya kuzindua ripoti hiyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Dk. Abdallah Posi amesema kwa mujibu wa Ripoti hiyo hali ni mbaya zaidi maeneo ya vijijini ambapo 74.7% ya watoto kote nchini wanafanya kazi hatarishi.

Akizungumzia Ripoti Hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania, NBS Dkt. Albina Chuwa amesema asilimia 92 ya watoto hao wanatumikishwa maeneo ya vijijini, ambapo pia matumizi ya muda kwa watoto ni asilimia 58.8 kujihudumia na asilimia 15.5 wakijisomea ukilinganisha na nchi nyingine kama Ghana ambayo 60.9% kujihudumia na 23.3 kujisomea.

Kwa upande wao mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, Azfar Khan, pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF Cecilia Baldeh wamesema, watoto milioni 168 wanatumikishwa duniani katika kazi mbalimbali hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha watoto kuondokana na umasikini unaochangia kujiingiza katika kufanya kazi mbalimbali.



Post a Comment

Post a Comment