Kauli ya Rais Barack
Obama ya kuwataka Wakristo kujua kuwa Uislamu si dini pekee
inayohusishwa na vurugu na mauaji, imezua kizaazaa duniani na baadhi
wameanza kuhoji kama kiongozi huyo wa kwanza mweusi wa Marekani ni
Mkristo.
Obama alitoa kauli hiyo
Jumatano wakati wa Siku ya Taifa ya Maombi (National Breakfast Prayer)
alipofananisha Vita vya Msalaba na vitendo vya ugaidi vinavyofanywa na
vikundi vya Kiislamu vyenye imani kali.
“Hadi tutakapokuwa juu
ya farasi na kufikiri kuwa jambo hili ni la pekee kwa baadhi ya sehemu,
kumbuka kwamba wakati wa Vita Vitakatifu (crusades) na Mahakama ya
Kanisa Katoliki (Inquisition), watu walifanya vitendo vya kutisha kwa
Jina la Kristo,” Obama alikaririwa na Shirika la Habari la AFP
akizungumza kwenye hafla hiyo Jumatano.
“Na katika nchi yetu, utumwa na sheria za kibaguzi (Jim Crow), zote pia zilihalalishwa kwa jina la Kristo.”
Obama alikuwa akitoa
hotuba yake kuhusu dini kwenye hafla hiyo iliyofanyika Washington, D.C.
Akitumia maandiko ya dini za Kiislamu, Kiyahudi na kikristo, Obama
alisifu imani yake.
“Utamaduni wa maombi
umetuweka pamoja, ukitupa nafasi ya kukusanyika kwa unyeyekevu mbele ya
Mungu na kutukumbusha nini kinatakiwa kushirikiana kama watoto wa
Mungu,” alisema.
Obama pia aliwageukia
magaidi wa kijihadi aliosema “wanaasi Uislamu”. Alilinyooshea kidole
kundi la Islamic State ambalo alisema “limefanya vitendo visivyoweza
kutamkwa vya ukatili “ Mashariki ya Kati pamoja na wanamgambo ambao hivi
karibuni waliua watu kadhaa kwenye ofisi za gazeti la vibonzo la
Charlie Hebdo nchini Ufaransa.
Lakini kauli yake imekosolewa sehemu mbalimbali.
Katibu wa Baraza la
Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Saba Raymond alisema
alichozungumzia Obama ni historian a hivyo dunia inatakiwa ijifunze.
“Kama kimetokea,
kimetokea. Tunatakiwa kujifunza kutokana na kilichotokea. Katika
ulimwengu wa sasa ni fursa ya kujifunza yale yaliyotokea na hayafai na
wakati huu yasitokee tena... wale wanaoyataka, washindwe,” alisema Padri
Raymond
Padri Raymond aliongeza
kusema: “Utumwa ulikuwa haufai na Marekani walijihusisha kwa hili
(kuuondoa) na hii ni historia ambayo wanapaswa kuiacha.”
Profesa wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe, George Shumbusho alisema:” Ni kauli ya kujihami na anaogopa
kuwanyooshea kidole moja kwa moja... Wamarekani wasingependa yatokee
kama yaliyowahi kutokea huko nyuma.
Post a Comment