Vitendo vya kibaguzi ambavyo vimetawala kisiwani Pemba tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio, sasa vimeanza kuonekana maeneo ya vijijini kisiwani Unguja.
Hali ya kubaguana imekuwa ikikua tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio ulioipa CCM ushindi kwenye visiwa vyote viwili baada ya CUF kuususia kutokana na kutokubaliana na kitendo cha Tume ya Uchaguzi (ZEC) kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani kwa maelezo kuwa sheria na kanuni zilikiukwa, jambo ambalo CUF ililipinga ikisema uchaguzi ulikuwa huru na haki na waangalizi wote walithibitisha hilo.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi huo wa marudio uliofanyika Machi 20, hali ya kutoelewana miongoni mwa wananchi imekuwa ikitawala kwenye kisiwa cha Pemba, ambako ni ngome ya CUF.
Wananchi wamekuwa wakibaguana kwenye vyombo vya usafiri, elimu, misikitini na kwenye biashara.
Hivi karibuni Mwananchi, iliandika makala kuhusu hali ya ubaguzi kwenye kisiwa cha Pemba, ikizungumza na wananchi na viongozi ambao walithibitisha kuwa ubaguzi unazidi kukua na kuvitaka vyama vya siasa kuzungumza na wanachama wao ili kuondoa hali hiyo.
Mwananchi imebaini kuwa hali hiyo ya ubaguzi imeanza kusambaa pia maeneo ya vijijini kisiwani Unguja.
“Kile kinachotokea Pemba ni cha mtoto. Hapa Unguja, kuna fukuto linafukuta chini kwa chini,” alisema naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar, Ali Ahmed Mazrui.
“Ipo siku litaibuka baya maana ni kama bomu. Kwa sababu wananchi bado wana donge rohoni.”
Mwananchi iliyotembea maeneo ya Nungwi, Mkokotoni na Matemwe yaliyoko Kaskazini Unguja, takribani kilomita 30 kutoka mjini ilishuhudia vitendo hivyo.
Mwananchi ilitembelea Mkokotoni ambako kuna usafiri wa boti au mashua za kuvuka kwenda Tumbatu na kuongea na wananchi ambao walithibitisha kuwepo kwa vitendo vya kubaguana.
“Ukitaka kwenda upande wa pili (Tumbatu) kama wewe ni mgeni, utapanda chombo chochote kiwe cha CUF au CCM, lakini kama wewe ni CCM au CUF itakupasa upande chombo cha wafuasi wenzako,” alisema kada wa CCM, aliyejitambulisha kwa jina Said Shaali.
“Mbaya zaidi, watu hawa (CUF) wameingiza siasa za chuki hadi katika misiba, hatushirikiani. Kuna siku mwanangu alifukuzwa na CUF kama mbwa alipokwenda kushiriki msiba wa rafiki yake kisiwani Tumbatu,” alisema Shaali.
Alisema hali hiyo ilianza kujitokeza baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mwaka jana, akidai kuwa wafuasi wa CUF walianzisha chuki dhidi ya wenzao wa CCM.
Ally Khatibu Juma, ambaye alisema ni nahodha wa boti inayosafirisha abiria kati ya Tumbatu na Mkokotoni, alisema si lazima kila mtu apande boti yake.
“Kila boti ina bendera ya chama, mimi yangu inapeperusha bendera ya CUF. Kamwe sitakuja kubeba mtu wa CCM. Ni bora niende na abiria wawili,” alisema Juma.
Alisema hata viongozi wa Serikali wakienda Tumbatu kupeleka msaada, haupokelewi.
“Viongozi wa Serikali wasijisumbue kutuletea msaada,” alisema.
“Siku moja mwakilishi wa jimbo la Tumbatu (CCM), Haji Omar Kheir alimtuma mtu aje atuletea tende katika misikiti mitatu, tulimkatalia kwa sababu ni haramu kwetu.”
Kauli hiyo ya Shaali ilithibitishwa na katibu wa CCM wa Wilaya ya Unguja Mjini, Baraka Shamte ambaye alisema baadhi ya misikiti ilikataa tende zilizopelekwa na Kheir ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Vikosi vya SMZ na Idara Maalumu.
Alisema kitendo kinachofanywa na CUF si kizuri na kwamba anashangaa kwanini mamlaka husika haioni mambo hayo ili chama hicho kichukuliwe hatua za kisheria kwa uvunjifu wa haki za binadamu.
Nungwi
Hali ni tofauti kwenye eneo la Nungwi ingawa kuna dalili za ubaguzi kuanza kuingia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wafuasi wa CUF wanaoishi Nungwi walisema kamwe hawawezi kumsamehe Jecha kwa kitendo chake cha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
“Hatutamsamehe Jecha kwa kitendo chake cha kuzima ndoto ya chama chetu kupata kiongozi ambaye ni chaguo la watu (Maalim Seif),” alisema Sharif Ali Sharif.
Sharif alisema chama hicho, hakina mpango wa kufanya vurugu kama watu wanavyodhani, ila njia sahihi wanayoitumia ni kutoshirikiana na watu wa CCM kuanzia Serikali hadi wanachama wake.
Alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ilimaliza matatizo ya Wazanzibari, lakini Jecha akishirikiana na Serikali wamefanya kila liwezekanalo kuhakikisha Maalim Seif anakwaa kisiki katika uchaguzi uliopita
“Wakitaka mkakati uishe ni haki
kutendeka na haki yenyewe itendeke kwa Maalim Seif kuwapo madarakani na si vinginevyo,” alisema Sharif.
Lakini mjumbe mmoja katika uongozi wa Shehia ya Nungwi alisema wafuasi wa vyama hivyo viwili sasa wanashirikiana kwenye shughuli za kijamii.
Sheha huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Khatib Kombo Bakari, alisema ikitokea msiba au sherehe wafuasi wa CCM hujumuika pamoja na wenzao
wa CUF bila tatizo lolote.
“Hapa hakuna suala kama hili,” alisema lakini akaonya: “Ila kuna watu wanataka kuiga mkakati huo ulioanza katika maeneo mengine.”
Alisema kuna baadhi ya watu wanataka kuiga mkakati huo, lakini bado hawaungwi mkono na wenzao na hadhani kama watafanikiwa.
Wakizungumzia kauli hizo, wanachama wa CUF walisema makada hao wanaogopa kusema ukweli kwa kuhofia kushughulikiwa na viongozi wa ngazi ya juu.
“Kwanza hii ni ngome ya CUF. Kwa hiyo mkakati huu upo na wasijisumbue hata kuja kuoa kwetu hatuwapi mke na waende wakawaoe CCM wenzao,” alisema Mwakahanzi Juma.
Aliongeza kuwa msiba ukitokea CCM wanakuwa mstari wa mbele kuhudhuria lakini wanachama wa CUF hawaridhiki badala yake wanaamua kuwatenga na mwisho wa siku wenyewe wanajisikia aibu na kuondoka eneo hilo.
Pemba ubaguzi balaa
Wakati hali ikianza kujitokeza kisiwani Unguja, ubaguzi unazidi kukua Pemba.
Shehia ya Kigomani, eneo la Matemwe, Hobe Juma Simai alisema CUF wanaendesha mpango huo wa kubaguana, lakini akasema hauna tija zaidi ya kurudisha nyuma maendeleo.
“Dai lao kubwa ni kwamba wamedhulumiwa haki yao. Ndiyo maana wakifika msikitini wakimuona imamu anayeswalisha ni CCM wanagoma kuswali.
“Mimi nawasihi warudi ili tuwe kitu kimoja na tushirikiane kwa maendeleo ya Shehia ya Kigomani na sehemu nyingine,” alisema Simai.
Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa CUF wanaoishi Kigomani walipinga kauli ya Simai ya kuwataka kuwa kitu kimoja na badala yake walisema hawatarudi nyuma.
Wafuasi hao walisisitiza kuwa endapo wakishirikiana na CCM watakuwa wamewasaliti wenzao kwa kuwa dhuluma wanayodai ilifanyiwa na CCM ni kubwa.
“CCM wanajisumbua, CUF hatutarudi nyuma, ndiyo maana sasa sasa hivi tunaswali kivyetu vyetu katika misikiti na tumeshajipangia ratiba waanze wao au sisi kuswali,” alisema Ramadhan Tano.
Mkazi mwingine wa Kigomani, Mcha Abdulrahman Kundi alisema si katika ibada hata kwenye masoko wakiona anayenadi bidhaa ni mtu wa CCM, hawampi ushirikiano.
“Wenyewe wanapenda sana tushirikiane, lakini sisi hatutaki. Kwa sababu ya dhuluma waliyotufanyia mwaka jana kupitia kwa Jecha Salum,” alisema Kundi.
Post a Comment