Bajeti 2016 /2017

Mjadala wa bajeti umetawaliwa na ubinafsi wa wabunge

Kesho ndiyo mwisho wa siku sita za mjadala wa bajeti kuu kwa mwaka wa fedha 2016/17, hoja kubwa iliyojadiliwa na wabunge kwa taribani siku nne ni kusudio la Serikali la kuondoa msamaha wa kodi kwenye kiinua mgongo cha wabunge watakapofika ukomo wa kukitumikia chombo hicho.

Utaratibu wa Bunge unaelekeza siku itakaposomwa bajeti kuu, siku inayofuata inakuwa mapumziko kuwapa muda wabunge kuisoma, kuichambua, kulinganisha kilichowasilishwa na matatizo ya majimboni kwao, wilaya zao, mikoa yao na masilahi ya taifa kwa ujumla.

Pia, wabunge hawakatazwi kuunda vikundi vya kujadiliana kwa kuichambua bajeti kwa pamoja na kujua maeneo ya kuchangia wakati wa mjadala bungeni, hatuwezi kujua siku hiyo wanayopewa wanaitumia vipi. Lakini, baada ya siku moja ya kujisomea, utaratibu mwingine ni mjadala uliotengewa siku sita kwa ajili ya wabunge kutoa hoja za kuisaidia Serikali kutumia vizuri fedha za walipa kodi na kubuni vyanzo vipya vya mapato.

Mapato makubwa ya Serikali yanatokana na kodi za wananchi na wawakilishi wa wananchi bungeni ni wabunge, hivyo, jukumu kubwa la mbunge ni kumwakilisha aliyemtuma hata vyama vya siasa vilivyotumiwa na wabunge kupata ubunge, ilani zake zinazungumzia kumkomboa mwananchi.

Kinachoshangaza hadi mjadala wa bajeti unakaribia ukingoni, wabunge waliopata nafasi kuchangia wengi wamejikita kupinga na kumtupia lawama Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango aliyewasilisha hoja hiyo, huku wengine wakimtuhumu amefikia uamuzi huo kwa vile yeye hana jimbo kwa sababu ni mbunge wa kuteuliwa na Rais.

Hoja zingine za bajeti zilizoguswa juu juu ni mgawo mdogo wa fedha kwenye ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huduma za utalii, tozo za usajili wa pikipiki na ongezeko la kodi kwenye mitumba.

Tunachokiona hapa ni ubinafsi zaidi, wabunge hawa wameghadhibika na kusudio la Serikali la kuondoa msamaha wa kodi kwenye kiinua mgongo chao, kwa maana nyingine kisu kimegusa mfupa, hatuoni kama wabunge hawa wanawatendea haki waliowapigia kura.

Hii ni bajeti ya kwanza kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, ni kiongozi aliyejipambanua amekuja kuinua uchumi wa nchi siyo wa wabunge, taifa haliwezi kujitegemea bila kupunguza utegemezi na kuongeza vyanzo vya mapato.

Ni wabunge hao hao wamekuwa wakiilalamikia Serikali kwa kuelekeza fedha nyingi kwenye matumizi ya kawaida na kutoa fedha kiduchu kwenye shughuli za maendeleo. Hiki kinachofanywa na wabunge ni ubinafsi kwa sababu mbunge mmoja alitoa hoja ya kupunguza fedha za kununulia mabehewa zipelekwe kwa CAG.

Kila mtu anajua kilio cha usafiri wa reli, ukosefu wa treni umeongeza gharama za maisha mikoani, lakini mbunge anatumia muda mwingi kutetea masilahi binafsi hadi anafikia kuona bora usafiri wa treni uendelee kuwa shida, lakini yeye masilahi yake yaendelee kuwa manono.

Mpango wa Maendeleo ya Taifa umeainisha mikoa mitano yenye umaskini ambayo yote inategemea usafiri wa reli ya kati, lakini hakuna mbunge aliyesimama kuzungumzia namna ya kuikwamua mikoa hiyo na umaskini. Tunadhani umefika wakati wabunge wetu kuthamini muda na waliowapeleka bungeni.

Mjadala wa bajeti haukuwa na afya hata kidogo, mawazo ya Serikali kwa asilimia kubwa yamebaki yale yale.

Post a Comment

Post a Comment