News

JINA LA LOWASSA LAZUA TAFRANI BUNGENI.BUNGE LAHAIRISHWA KWA MUDA

Jina la aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana liliibua sintofahamu Bungeni na kupelekea Spika wa Bunge, Job Ndugai kuingilia kati na kuahirisha kikao cha asubuhi.

Mvutano uliibuka Bungeni humo wakati Mbunge wa Jimbo la Madaba, Joseph Mhagama (CCM) kucha mada aliyokuwa akichangia kuhusu Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2015/16 hadi 2020/21, na kuzungumzia oparesheni ya kutumbua majipu inayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli.

Mhagama aliwatupia dongo wapinzani wanaounda Ukawa kuwa ni vigeugeu akieleza kuwa hivi sasa wanapinga zoezi la utumbuaji majipu, wakati hapo awali wao ndio walikuwa vinara wa kupinga ufisadi na ndio iliyokuwa sera yao.

Baada ya kauli hiyo ya Mhagama, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alisimama kutoa taarifa ambapo alimueleza kuwa Wapinzani hawapingi zoezi la kutumbua majipu kwa watendaji waliofanya makosa, huku akitoa mfano kuwa hata Wilson Kabwe (aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam) aliwahi kulalamikiwa Bungeni na aliyekuwa mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje.

Hata hivyo, Mhagama alikataa kuipokea taarifa hiyo na kuendelea kurusha makombora kwa wapinzani akitoa mfano wa jina la Lowassa ambalo lilizua hali ya sintofahamu.

"Siwezi kuipokea taarifa hiyo kwa sababu wapinzani hawa hawa ndio walioleta taarifa hapa Bungeni na kutuaminisha kuwa Lowassa ni fisadi, mwaka jana walimkumbatia na kumpa nafasi ya kugombea urais, alisema Mhagama.

Baada ya kauli hiyo, utulivu ulitoweka kwa muda na kutaka kutokea vurugu Bungeni hapo, hali hiyo ilisababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai kusitisha kikao hicho cha asubuhi, na kukiitisha tena jioni.

Post a Comment

Post a Comment